Monday, January 4, 2010

Watu 41 wala ugali wenye sumu


Watu hao walifikishwa hospitalini wakiwa taabani, wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Kigoma ya Maweni.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa Kigoma, Ramadhani Twaha aliwaambia waandishi wa habari mjini hapa jana kuwa watu hao walikumbwa na mkasa huo juzi mchana baada ya kula ugali huo ambao ulikuwa maalumu kwa ajili ya chakula cha mchana.
Kamanda Twaha alisema kuwa familia ya kwanza kuathirika na mkasa huo ni ya Hussein Omari iliyokuwa na watu 21 ambao walianza kupatwa na mkasa huo kuanzia majira ya saa nane mchana baada ya kuwa wamemaliza kula chakula hicho.
Amesema, watu hao wakati wanajipumzisha walijikuta wanaanza kupatwa na kizunguzungu na kutapika, walikimbizwa katika Hospitali ya Maweni kwa matibabu ambapo walipatiwa huduma.
Kamanda Twaha amesema, saa moja baadaye familia ya Maulid Sange iliyokula nayo ilianza kupatwa na tatizo hilo kwa ndugu hao kuanza kusikia kizunguzungu na kutapika ambao pia walichukuliwa na kukimbizwa hospitali ya Mkoa Kigoma Maweni kwa matibabu.
Amesema, Polisi mkoani Kigoma wamemkamata Stamili Kassim, mke wa Bukuru Matama mmiliki wa duka hilo ambalo watu hao walinunua unga hapo kwa uchunguzi zaidi.
Mmiliki wa duka hilo yuko safarini Mwanza kwa shughuli za kibiashara.
Kamanda huyo alisema sampuli ya mahindi yaliyotumika kutengeneza unga huo, unga na matapishi ya watu walioathirika na tukio hilo yamechukuliwa na kupelekwa kwa Mkemia wa Serikali Kanda ya Mwanza kwa uchunguzi zaidi.
Ofisa Muuguzi wa Hospitali ya Mkoa Kigoma Maweni Zuwena Gotta alithibitisha kufikishwa hospitalini hapo kwa watu hao na kusema kuwa hadi sasa watu 41 wameshafikishwa hospitalini hapo kutokana na kuathiriwa na ugali huo wenye sumu.

CHANZO: HABARILEO

No comments:

Post a Comment