Monday, January 18, 2010

HUPATI CHOO MARA KWA MARA? SOMA HAPA!


Ukosefu wa choo ni tatizo sugu la kiafya linalowakabili watu wengi, wengine bila kujua kama ni tatizo, huchukulia kuwa ni hali ya kawaida. Ukweli ni kwamba ukosefu wa choo ndiyo chanzo cha maradhi mengi, yakiwemo magonjwa ya moyo.

Ili mtu apate choo, angalau mara moja kwa siku, anahitaji kula vyakula vinavyosagika kirahisi tumboni. Vyakula hivyo ni vile ambavyo vina kiasi kikubwa cha kamba lishe na kiasi kidogo sana cha mafuta. Aina hii ya vyakula huwa muhimu sana, hasa kwa wale watu wenye matatizo ya kuumwa tumbo mara kwa mara.

Kwa kujijua hali hiyo na kuamua kula vyakula vyepesi, mgonjwa anaweza kupata ahueni haraka zaidi kuliko mtu anayekula vyakula vigumu. Si ajabu kuona wazee wanashauriwa kula aina hii ya vyakula kwa sababu mfumo wao wa usagaji chakula tumboni huwa hauna nguvu ya kusagaa vyakula vigumu.
VYAKULA RAHISI KUSAGIKA TUMBONI
Unapoenda sokoni au dukani kununua mahitajai yako ya chakula, ni muhimu sana kuzingatia ubora wa chakula ikiwa na pamoja na kuwa na sifa ya kusagika kirahisi tumboni. Kuna baadhi ya watu wanadai kwamba kutokana na hali halisi ilivyo, hakuna vyakula vingi vya kuchagua ili kukidhi haja hiyo, madai ambayo siyo kweli, kwani Mungu katujaalia vyakula bora vya kila aina:
MBOGA ZA MAJANI NA MATUNDA
Mboga za majani, hasa zile za rangi ya kijani kama kabichi, ni rahisi sana kusagika tumboni. Mboga za majani zina kiwango kikubwa cha vitamini na madini na husaidia sana katika usagaji wa chakula tumboni. Halikadhalika matunda ya aina mbalimbali, kama vile mapapai na embe, ni muhimu kuliwa. Mbali ya vyakula hivi kusaidia usagaji wa chakula, lakini pia ni lishe muhimu kwa kupunguza uzito.

WALI
Katika mlo wako wa kila siku, ambao unazingatia lishe bora, inashauriwa sana kujumuisha wali, tena kwa wingi. Mchele una virutubisho ambavyo husaidia mchakato wa usagaji chakula tumboni, hivyo kumuwezesha mlaji kupata choo kirahisi.

NYAMA YA KUKU
Nyama ya kuku nayo imo kwenye orodha ya vyakula vinavyosagika kirahisi tumboni. Lakini ni muhimu sana kujua ni aina gani ya nyama ya kuku unayotakiwa kula. Unapokula nyama ya kuku, hakikisha unaondoa ngozi na kula nyama pekee bila ngozi, ambayo huwa na mafuta mabaya yanayodhoofisha mfumo wa usagaji chakula tumboni.
NDIZI MBIVU
Miongoni mwa sababu kubwa zinazolifanya tunda hili liendelee kuwa maarufu duniani ni uwezo wake wa kurahisisha usagaji chakula tumboni. Utafiti wa kisayansi umethibitisha kuwa ‘vimeng’enyo’ vilivyomo kwenye ndizi huimarisha mfumo wa usagaji chakula tumboni. Hata watoto wachanga na wadogo wenye matatizo ya kuchafuka tumbo wanaweza kupewa ndizi mbivu kama tiba mbadala.

MAKATE WA TOSTI
Inaelezwa kuwa mkate wa tosti unasagika kirahisi sana tumboni kuliko kula mkate mkavu, hivyo unashauriwa kutosti mkate wako na kula kama kifungua kinywa na bila shaka hutasumbuliwa na ukosefu wa choo kama mtu anayekula mkate mkavu.

KIASI CHA MLO
Kiasi unachokula kwa siku ni miongoni mwa vitu vya kuzingatia linapokuja suala la usagaji chakula tumboni. Watu wengi hufanya makosa kwa kula na kushiba kupita kiasi na kujikuta wanakabiliwa na tatizo la ukosefu wa choo licha ya kula vyakula tulivyovitaja awali. Unashauriwa kula kiasi kidogo cha mlo kila baada ya muda, hata mara tano kwa siku, badala ya kula milo miwili mikubwa sana kwa siku.
MWISHO, jenga mazoe ya kula vyakula laini vinavyosagika kirahisi tumboni na epuka vyakula vinavyochangia ukosefgu wa choo. Vyakula vinachangaia kudhoofisha mfumo wa usagaji tumboni ni pamoja na vyakula vya kukaanga kwa mafuta mengi kama vile chips, vitumbua, mandazi, n.k. na ukosefu wa maji kunakosababishwa na mtu mwenywe kwa kutokunywa maji mengi kila siku.

No comments:

Post a Comment