Monday, January 18, 2010

Mchezaji Mweusi wa Marekani Abadili Rangi ya Ngozi Yake


Mmarekani mweusi Sammy Sosa ambaye aliwika sana enzi zake kwenye mchezo wa Baseball amebadili rangi ya ngozi yake kutoka nyeusi kuwa nyeupe kama mzungu.
Mchezaji maarufu wa zamani wa Baseball, Sammy Sosa mwenye umri wa miaka 41 amejibadilisha rangi ya ngozi yake kuwa mweupe kama mzungu kwa kutumia krimu za kujichubua.
Sosa alianza kujichubua kuanzia mwaka 2007 na wiki iliyopita alionekana kwenye tuzo za Latin Grammy jijini Las Vegas akiwa hana tena rangi yake nyeusi ya kuonyesha asili yake ya Afrika.
Sosa alionekana mweupe kama mzungu na kwa watu ambao hawamfahamu ni vigumu kuamini alikuwa mweusi 'tii' zamani.
Sosa amesema kuwa nia yake kubadili rangi ya ngozi yake ni kutokana na mapenzi yake mwenyewe na si kumuiga marehemu mfalme wa muziki wa Pop, Michael Jackson.
Sosa amekiri pia kubadilika kwa rangi hakutokani na maradhi yoyote ya ngozi bali ni kutokana na krimu anayoitumia ambayo alisema ataipigia kampeni za kibiashara.
Hivi karibuni idadi ya watu weusi wanaojichubua nchini Marekani ili wakubalike katika soko la wazungu imezidi kuongezeka na wataalamu wa ngozi wanaonya kuwa matumizi ya krimu kujichubua ni hatari kwa afya.
Magonjwa mengi ya ngozi kama vile kansa ya ngozi yamekuwa yakihusishwa na madawa na krimu za kujichubua.
 

No comments:

Post a Comment