Saturday, January 9, 2010

SIRI YA KUISHI MAISHA MAREFU


Ili mtu ainshi maisha marefu, kuna vitu vingi vya kufanya na kuzingatia wakati wote wa maisha yake. Utafiti wa kisayansi umegundua kwamba suala la mtu kuzeeka kutokana na vinasaba (genes) alivyonavyo, linachukua nafasi ya theluthi moja tu na theluthi zingine mbili zinategemea sana staili ya maisha anayoishi.
Staili hiyo ni pamoja na jinsi ambavyo unakula na aina ya chakula unachokila. Vile vile mazoezi yanachukua nafasi kubwa katika kuimarisha afya ya mwili wako. Halikadhalika, msongo wa mawazo (stress) ni mtihani mwingine unaopaswa kujua jinsi ya kuushinda unapokupata, kwani huathiri afya kwa kiasi kikubwa.
Kwa mujibu wa ripoti maalum ya Mabingwa wa Upasuaji nchini Marekani, kuhusu lishe na afya, asilimia 75 ya vifo vitokanavyo na ugonjwa wa moyo, asilimia 60 ya vifo vitokanavyo na magonjwa yatokanayo na saratani ya wanawake na asilimi 40 ya magonjwa yatokanayo na saratani ya wanaume, yanasababishwa na ukosefu wa virutubisho mwilini na lishe bora.
Utafiti huo umesisitiza kuwa vifo vingi vingeweza kuepukwa iwapo watu wangejali afya zao ipasavyo. Katika hili, utaona kwamba umri wa mtu kuishi unatofautiana kati ya nchi moja na nyingine kutokana na kuwa na tofauti za kitamaduni na staili za maisha za watu wa nchi hizo.
Inaelezwa kwamba, raia wengi wa nchi za Kilatini hawaendi sana hospitali, lakini wanaishi maisha marefu na ni raia wachache sana wanaokufa kutokana na ugonjwa wa moyo, saratani au kiharusi. Hii ni taarifa njema kwa watoa huduma ya afya wengine, lakini Walatino wamewezaje kuwa hivi?
Wachambuzi wengi wa masuala ya kuishi maisha marefu wanaihusisha hali hii na tabia ya Walatini kuheshimu familia, kuzingatia maadili ya kazi, dini na mpangilio mzuri wa maisha ya kijamii.
Kuwa na familia imara na jamii yenye kuelewana huchangia kwa kiasi kikubwa mtu kuishi maisha marefu. Tunahitaji kuoanisha maisha yetu ya kila siku kati ya kazi na kujumuika na jamii kila siku. Tamaduni za kilatini zina fursa nyingi za kujumuika kati ya familia moja na nyingine na hata na wageni.

LISHE YA WALATINI
Mbali ya kuwa na maisha ya kijamii mazuri na kuzingatia suala zima la kupumzika baada ya saa za kazi, lishe ya Walatini wengi huzingatia sana mahitaji ya mwili na kanuni za afya. Walatini wanakula sana samaki, mboga mboga, jibini na mikate. Nyama nyekundi huliwa kwa kiasi kidoga sana miongoni mwao.
Hupenda kula chakula kidogo kidogo kila wakati, kiasi cha mara tano kwa siku. Katika kipindi hicho, hula aina mbalimbali ya vyakula asili vilivyotengenezwa kutokana na nafaka, matunda, mboga za majani na hupenda sana kufanya mazoezi.
Kukamilisha makala yote kwa ujumla, zingatia mambo yafuatayo ili kufikia kilele cha kufaidi maisha marefu yenye afya bora:
Epuka unene, kwani kuwa mnene siyo afya, mara nyingi unene huambatana na magonjwa ya moyo, kisukari n.k. Fanya mazoezi mara kwa mara, bila kusahau kuchua mwili mzima (body massage) ambako kumeelezwa huboresha kinga ya mwili.

Pata muda wa kupumzika, kwasababu kulala na kupata usingizi mzuri ni sehemu ya kanuni za afya bora. Sambamba na hilo, kama una nafasi, nenda safari ya mapumziko katika sehemu ambayo utapata muda wa kupumzika na kukaa katika mazingira yenye utulivu.
Mwisho kabisa, suala la kujamiina lisisahaulike. Inaelezwa kwamba, tendo la ndoa humuondolea mtu msongo wa mawazo na kumfanya aonekane kijana, kwani tendo hilo linapofanyika, hutoa kirutubisho aina ya ‘endorphins’ ambacho hushusha kiwango cha msongo wa mawazo. Hii haina maana kwamba uzini, oa mke na kama ni mwanamke olewa!

No comments:

Post a Comment