Tuesday, March 9, 2010

Bibi wa China Aota Mapembe Kama Mbuzi

 Bibi mwenye umri wa miaka 101 wa nchini China anawashangaza mamia ya watu kutokana na mapembe kama ya mbuzi yanayoendelea kujitokeza kwenye kichwa chake.
Bibi Zhang Ruifang mwenye umri wa miaka 101 wa kijiji cha Linlou katika jimbo la Henan nchini China alianza kuota pembe moja kwenye kichwa chake mwaka jana.

Hadi sasa pembe hilo lililoota kwenye upande wa kushoto wa paji lake la uso limekua na kufikia urefu wa sentimeta sita. Upande wa kulia wa paji lake la uso kuna pembe jingine ambalo ndio kwanza linaanza kujitokeza.

Familia yake imepagawa na mapembe hayo na haijui kwanini yanajitokeza kwenye kichwa chake.

Mtoto wa mwisho wa bibi huyo anayeitwa Zhang Guozheng mwenye umri wa miaka 60 alisema kuwa wakati mapembe hayo yalipoanza kujitokeza mwaka jana hawakujali sana walidhania ni makunjamano ya ngozi tu.

"Lakini siku zilivyozidi kwenda pembe lilijitokeza kwenye kichwa chake na sasa limefikia sentimita sita" alisema Zhang ambaye kaka yao wa kwanza ana umri wa miaka 82.

"Hivi sasa kuna kitu kinajitokeza kwenye upande wa kulia wa paji lake la uso bila shaka ni pembe jingine", aliendelea kusema Zhang.

Madaktari walisema kuwa mapembe hayo yanaweza kuondolewa kwa operesheni lakini sababu ya kujitokeza kwa mapembe hayo bado haijulikani.

No comments:

Post a Comment