Habari zaidi zinasema BoT imesitisha nyongeza ya mikopo ya nyumba ya asilimia 50 iliyoidhinisha kwa wafanyakazi wake, hatua ambayo imekuja siku chache baada ya kuidhinishwa na menejimenti ya taasisi hiyo kubwa ya fedha.
Taarifa za matumizi hayo makubwa ya fedha hizo za walipakodi katika kujenga makazi ya gavana ziliripotiwa na Mwananchi Ijumaa iliyopita katika habari iliyoeleza jinsi nyumba ya kigogo huyo wa BoT ilivyogharimu Sh1.4 bilioni kuikarabati, kabla ya Ndulu kutoa ufafanuzi kuwa nyumba hiyo ilijengwa upya na si kwamba ilikarabatiwa.
Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano juzi, Mkulo alisema pamoja na kushtushwa na taarifa hizo, jambo hilo ni kubwa na linahitaji umuhimu wa kipekee kuchunguzwa ili walipakodi wajue ukweli wa matumizi ya fedha wanazoilipa serikali.
"Lazima tuchunguze ukweli wa taarifa hizo, maana hili ni jambo kubwa na linamhusu mtu mkubwa," alisema Mkulo katika mahojiano na gazeti hili.
Mkulo alisema kuwa alikuwa safarini nje ya nchi na kwamba baada ya kurejea nchini juzi, ofisi yake itatumia wiki hii kufanyia uchunguzi suala hilo na wiki ijayo atakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuweka mambo yote hadharani.
Akitoa ufafanuzi wa tuhuma hizo wiki iliyopita, licha ya kukiri matumizi hayo ya fedha, Profesa Ndulu alisema kuwa nyumba anayoishi ilianza kujengwa kutoka chini na kwenye kiwanja ambacho ni cha BoT.
"Nyumba haijakarabatiwa, imejengwa from the ground (kutoka chini)... ni tofauti kukarabati na kujenga nyumba mpya... huu ni upotoshaji wa wazi na kujaribu kuchafua mema," alilalamika gavana huyo.
Aliongeza: "Napenda taarifa sahihi ambazo hazipotoshi ukweli kwa maana taarifa kama hizo zinaharibu kila kitu, kizuri na kujenga taswira mbaya kwa wananchi, kitu ambacho si sahihi."
Mwananchi toleo la Desemba 23, mwaka huu iliripoti kuwa nyumba anayoishi sasa gavana huyo ilikarabatiwa kwa takriban Sh1.4 bilioni na kwamba ilikuwa kwenye mradi wa kukarabati nyumba za vigogo wanne wa BoT; ya Ndulu na manaibu wake watatu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, nyumba nyingine ni pamoja na aliyokuwa akiishi gavana wa zamani, marehemu Daudi Balali ambayo Prof Ndulu alidaiwa kuikataa kwa kuwa haina bwawa la kuogolea.
Licha ya tuhuma hizo, BoT inalalamikiwa kwa kujiidhinishia mamilioni ya fedha za mikopo yenye tofauti kubwa ya viwango baina ya wafanyakazi wa chini na vigogo.
Katika hatua nyingine, BoT imesimamisha nyongeza ya mikopo ya nyumba kwa asilimia 50, ambayo menejimenti hiyo iliridhia nyongeza yake ambayo watumishi wa kada ya chini wangejipatia mkopo wa hadi Sh30milioni na vigogo hadi Sh100milioni.
Habari zilizolifikia Mwananchi na kuthibitishwa na Gavana wa BoT, Profesa Ndulu zimethibitisha kusimamishwa kwa mikopo hiyo.
Kabla ya kusimamishwa kwa mikopo hiyo baadhi ya watumishi wa taasisi hiyo walikaririwa na vyombo vya habari (siyo Mwananchi), wakilalamika kuwa nyongeza hiyo ililenga kuwanufaisha zaidi vigogo.
Walidai kuwa matarajio yao yalikuwa wafanyakazi wa kawaida wangepewa kipaumbele zaidi, lakini hali ikawa kinyume.
Kusimamishwa kwa mikopo hiyo pia kumeibua mitazamo tofauti kwa wafanyakazi wa taasisi hiyo, wengi wakionyesha mashaka kwa hatua hiyo wakidai inawaaminisha kuwa nyongeza hiyo ilikuwa na lengo la kuwanufaisha zaidi wakubwa.
"Hii inaleta mashaka kwani kama hapakuwa na tatizo ni kwa nini baada tu ya kuripotiwa kwenye vyombo vya habari ndipo ikasimamishwa?" alihoji mmoja wa wafanyakazi wa benki hiyo.
"Sina hakika sana juu ya sababu zilizofanya mikopo hiyo isimamishwe na hatua au marekebisho yanayokusudiwa kuchukuliwa, lakini hii inaweza kutoa picha kuwa kuna mambo hayakuwa sawa ndio sababu imesimamishwa baada ya vyombo vya habari kuiripoti."
Lakini juzi, Gavana Ndulu alisema lengo la kusitisha mikopo hiyo ni kutoa elimu zaidi kwa wafanyakazi hao kuhusu mikopo hiyo.
Alisema imebainika kuwa wafanyakazi hao hawakuwa na elimu ya kutosha kuhusu vyongeza hiyo ya viwango vya mikopo na kwamba ndio maana walikaririwa na vyombo vya habari wakilalamika.
Ndulu alifafanua kuwa upo umuhimu wa elimu hiyo kwa wafanyakazi ili wasije wakabeba mzigo wasiouweza kwa kuwa mikopo hiyo ina masharti mengi kwa mkopaji.
"Tumeongeza masharti mengi na hatutaki mtu abebe mzigo asiouweza. Tumegundua wafanyakazi wengi hawakuelewa na ndio maana tumeona kuna umuhimu wa kuelimishana kwanza," alisema Prof Ndulu.
"Pengine elimu ilipaswa itangulie kwanza. Mara nyingi hivi vitu ni kuelewana. Ilionekana wengi hawakuelewa ndio sababu wakalalamika kwenye vyombo vya habari. Kwa hali hiyo sasa tumeisimamisha mikopo hiyo kwanza na tayari nimewaagiza maofisa husika kusimamia utaoaji wa elimu hiyo."
Gavana Ndulu alisema mfuko huo wa mikopo kwa nyumba umekuwepo kwa muda mrefu na kwamba kilichofanyika ni kuongeza tu viwango vya mikopo ili kuendana na mabadiliko ya hali ya maisha.
Kuhusu chanzo cha pesa hizo, alisema si za serikalini bali zinatokana na operesheni mbalimbali za benki hiyo ikiwa ni pamoja na riba inayotokana na mikopo mbalimbali wanayoitoa kwa serikali na kwa mabenki mengine nchini.
Kuhusu masharti ya mikopo hiyo alisema inapotokea mtumishi amestaafu kabla ya kumaliza kurejesha mkopo huo, basi sehemu ya mafao yake hutumika kufidia kiasi kilichosalia.
BoT imekuwa ikiangaliwa kwa karibu tangu kuibuka kwa kashfa ya wizi wa zaidi ya Sh133 bilioni kwenye Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA).
Taasisi hiyo pia imekumbwa na kashfa nyingine kama za bima ya maghorofa yaliyo jijini Dar es salaam na Zanzibar, kuongeza gharama katika uchapishaji wa noti na matumizi mabaya ya madaraka katika ujenzi wa maghorofa pacha.
Wafanyakazi wa benki hiyo pia wamejikuta kwenye kashfa za kufanikisha njama za wizi, kuajiriwa kwa kutumia vyeti vya kughushi na tuhuma za watoto wa vigogo kupewa ajira za upendeleo.
CHANZO: MWANANCHI
ERIC CHELLE ATANGAZWA KOCHA MPYA TIMU YA TAIFA NIGERIA
39 minutes ago
No comments:
Post a Comment